Kwa Nini Tumesilimu?

Converts Panel: Why We chose Islam | UNSW Islamic Awareness Fortnight 2011, Sydney



 Nichole Arel
Safari Kuelekea Kwenye Ukweli Wa Milele Je, Kweli Ni Dini Ya Waarabu?


Mara nyingi hujikuta nikiwaza jinsi nilivyobarikiwa. Maisha ninayoishi sasa ni tofauti sana na niliyotarajia kuishi mwaka mmoja uliopita, fikra zangu za mwanzo niamkapo asubuhi, njia yangu ya kufikirika katika maisha, na hususan moyo na roho yangu. Kamwe nisingeota kwamba ndani ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja maisha yangu yangeelekea kwenye njia hiyo isiyotarajiwa. Sio hilo tu. Njia ninayopita sasa inanipeleka kwenye barabara ambazo sikujua kama zipo. Kwa kweli pale unapoanzia safari yako bila shaka sio kiashiria hata kidogo cha mahali utakapo kamilishia safari yako.

Nikiwa kama mtoto, nilitamani sana kupelekwa kanisani. Hisia ya kujumuika na watu na kuabudu iliiteka akili yangu. Nilitamani sana kuwa karibu na Mungu kabla hata sijaunda fikra hizo katika akili yangu mwenyewe. Kitu kisichoeleweka kiliipeleka roho yangu katika hamasa kubwa, kiasi kwamba nilifanya mazoea ya kumuamsha baba yangu kila siku ya Jumapili kwa kumuomba anipeleke kanisani.

Kwa bahati mbaya familia yangu ilifanana sana na familia za Wakristo wa Kimarekani wa hali ya kawaida, wanaoridhika kujiita wanadini kwa misingi ya mahudhurio yao ya mara mbili kwa mwaka katika misa ya Kikatoliki. Wakati wa Krismasi na Jumapili ya Pasaka. Hivyo nilikulia katika mazoea ya kusikia maneno yafuatayo: “sio leo, labda wiki ijayo”. Kwa huzuni kubwa, ningerudi chumbani nikiwa nimenuna na kusubiri Jumapili nyingine ifike, ili nisikie maneno hayo ya kusikitisha yakijirudia tena na tena.

Huo ulikuwa ni usumbufu wa siku zote ambao haukuniacha kamwe kadiri nilivyojitahidi kuuondoa.

Kadiri nilivyosonga mbele kiumri, nilijifunza kuacha kutoa maombi yangu kwa baba yangu kutokana na jitihada zangu zote kugonga mwamba. Nikaridhika kuutumia muda wangu wa ziada katika kujisomea katika hali ya upweke, hususan vitabu vinavyo zungumzia tamaduni na dini mbalimbali ulimwenguni. Niliposoma zaidi kuhusu historia ya dini yangu, Ukatoliki, nilikerwa na jinsi inavyolaani watu kuhoji mafundisho yake. “Hakika hii haiwezi kuwa madhehebu sahihi ya Ukristo”, niliwaza.

Muda ulisonga mbele na bado sikuwa nimepata dini inayo onekana kuzungumza na moyo wangu. Labda nilikuwa nikitaraji kupata kitu cha kuchochea hisia zilezile nilizokuwa nazo kuhusu kanisa nilipokuwa mtoto, ingawa nilijua kwamba hili lilikuwa ni takwa la kijinga. Mfarakano na dini huanza pale tu mtu anapoanza kuelewa madai na hitilifu za dini hizo.
Sikuweza kuifunika akili yangu dhidi ya madai ya Imani ya Utatu kwa namna yoyote ile niliyojaribu kufanya hivyo. Sikuelewa kwa vipi nilitakiwa kuamini nadharia na mafundisho yasiyoeleweka wala kuingia akilini. Nilichukia kuona kwamba mantiki ilionekana kutokuwa na nafasi katika Ukristo na kitendo cha kuhoji na kujadili mafundisho ya dini hiyo kilichukuliwa kuwa ni alama ya imani dhaifu. Sasa ni kwa sababu gani Mungu alimpa mwanadamu uwezo wa kutumia busara?

Kwa kweli niliachana nayo yote na kukubali kwamba kamwe nisinge weza kupata ukweli. Nilijiengua kuamini kwamba alikuwepo Mungu lakini wanadamu wasingeweza kamwe kumjua au kuijua dini ya kweli imfaayo mtu mpaka tutakapo kutana naye siku moja.
Niliishi miaka mingi nikiwa na imani hii mpaka hivi karibuni kitu kisichoelezeka kilipokuwa kikinisukuma tena kutafuta ukweli. Msukumo huu takriban ilikuwa ni sauti lakini isiyokuwa katika maana ya kawaida. Ni sauti iliyo nisukuma mara kwa mara ambayo haikuniacha hata kidogo ingawa nilijitahidi sana kuiondosha.

Hivyo moja kwa moja nilinunua Biblia ili nisome, nikidhani kuwa lazima ukweli utakuwa umejificha katikati ya kurasa za kitabu hicho. Uwenda nitakuwa niliukosa katika kipindi cha miaka yote hiyo iliyopita. Jambo hili liliniweka karibu zaidi na ukweli kuliko nilivyowahi kuhisi.

Nilipokuwa nikiisoma Biblia nilipatwa kuvutwa na matukio yaliyokuwa yakitokea ulimwenguni wakati huo. Nilijikuta nikitumia muda wangu wote wa ziada kufululiza kuandika barua kwenda kwa maafisa wa serikali yangu kutetea haki za Wapalestina na Wasudani, vile vile nikipinga vita mbalimbali vinavyo endelea duniani kote, na kudurusu juu ya madhehebu mbalimbali ya Kikristo.

Nilipanga kwenda kufanya kazi za kujitolea nchini Palestina kama ningeweza kukusanya pesa za kunifikisha huko. Kwa kawaida, kutokana na ghasia katika eneo hilo na mipango yangu ya safari, niliona ni muhimu kusoma mambo mbali mbali kuhusu Uislam na kuifahamu dini ya watu hao niliotaka kuwasaidia.

Nilivutiwa sana na nilichokisoma kuhusu dini na imani ya Waislamu. Nadharia ya Mungu Mmoja badala ya utatu, kuwaheshimu na kuwatukuza Mitume na Manabii wote kitu ambacho sikukiona katika Biblia, vielelezo vya Kisayansi vinavyotolewa na Qur’an, vipengele vyote vinavyo uzunguka Uislamu, heshima kwa akina mama, utakatifu wa familia. Hii ni dini pekee niliyowahi kukutana nayo ambayo inakubaliana na akili na busara na bado ikaendelea kuwa na miujiza tele ya Mungu.

Lakini Uislamu ni dini ya Waarabu, kweli?
Vijana wa kike wa Kimarekani hawawezi kuvutika nayo, je yawezekana? Baadaye niligundua kwamba Uislamu ndio dini inayokua kwa kasi zaidi duniani, kwa kiasi kwamba Waislamu wengi sio Waarabu, na kwamba miongoni mwa watu wanaoingia kwa kasi zaidi katika Uislamu katika Ulaya ni kundi la wanawake wenzangu wa kizungu tunaoishi katika eneo moja.
Wazo hasa la kuupa kisogo Ukristo, bila kujali ni kwa jinsi gani dini hiyo ilivyoendelea kuwa na umuhimu mdogo kwangu, lilikuwa ni wazo la kuogofya na la kukanganya. Niliamua siku za Jumapili kwenda katika kanisa lisilokuwa na mrengo wa kimadhehebu na kuutumia muda mwingi kusoma Biblia. Nilisali na kuomba kwamba nipate kile nilichokuwa kikikitafuta lakini yote niliyokutana nayo yalizidi kunikanganya zaidi na zaidi. Bado sikuweza kukubaliana na imani ya Utatu na nilishtuka sana kwamba sikuona hata ukurusa mmoja katika Biblia ambapo Yesu alidai kuwa ni Mungu.

Kwa vipi tuliweza kufikiria kwamba Mungu aje ardhini na kufa kwa ajili ya dhambi zetu? Ningewezaje kuelezea mifano inayoshtusha ya mafundisho ya Ukristo yanayo fanana kabisa na ngano za kipagani za wakati wa kipindi cha ueneaji wa Ukristo enzi za Himaya ya Rumi? Vipi kuhusu madai ya Ukristo kwamba tunaweza kuishi namna tutakavyo na bado tukaingia peponi kwa kumuamini tu Yesu? Kama yesu alidaiwa kuwa ni Mungu aliyejibadilisha katika sura ya mtu, kilio alichokitoa kwamba Mungu alikuwa amemuacha kilikuwa na maana gani? Kurasa zisemazo kwamba Yesu angemtuma “Mfariji” baada yake zilimkusudia nani? Nani “Roho wa Kweli” aliyetabiriwa kuja baada ya Yesu?

Nilisongwa na maswali yaliyonikera na kukubali yasiyoweza kuepukika. Nilipoanza kufanya kazi, nilisali na kumuomba Mungu anionyeshe njia ya dini ninayo takiwa kuifuata. Je kama nilitakiwa kuwa Mwislamu Mungu angenitumia alama?

Nilichukua mkoba wangu na kuelekea chini kwenye gari yangu katika eneo la kuegesha magari. Kwa mshangao, palikuwa na mwanamke wa Kiisalmu aliyesimama kando ya gari yangu wakati akitafuta funguo zake. Je hii yaweza kuwa ndio alama niliyoomba? “Haiwezekani”, akili yangu ilisema, lakini nikaamua kutopoteza fursa hii hivyo nilimkaribia.
“Binti, naweza kukuuliza kitu? Wewe ni Mwislamu, ni kweli?” Alionekana kushtuka kwa sababu alikuwa amesubiri kusikia wazo la kijinga la aina moja lililozoeleka miongoni mwa watu ambao, kwa wastani, hawana maarifa ya tamaduni au dini mbalimbali, “Ndiyo, Mimi ni Mwislamu” alijibu. Nikamuuliza iwapo alikuwa akisali katika msikiti niliokuwa nikiufahamu. Nilimueleza kwa mukhtasari kwamba Uislamu unaonekana kuwa dini pekee inayoingia katika akili yangu. Alisisitiza kwamba niende kwenye msikiti ulio katika njia ielekeayo nyumbani kwangu lakini nikamueleza kuwa nilitaka kwanza kuidurusu na kuisoma Qur’an.

Nikiwa ninaendesha gari yangu kuelekea nyumbani nilijikuta nimeegesha mbele ya msikiti huo. Papo hapo nikawaza kuwa hiyo yaweza kuwa alama nyingine lakini, kwa mara nyingine, akili yangu ilikataa kuamini. Nilikwenda mpaka kwenye mlango nikitetemeka kama jani ambapo niliazimia kurudi garini kwangu na kwenda nyumbani haraka iwezekanavyo. Lakini badala yake miguu yangu ilinipeleka mbeli, bia kutilia maanani amri ya ubongo wangu.

Baba yangu alinimbia kwamba mimi nilikuwa mfu kwake na hivyo nisiwasiliane naye tena.
Nilipopata njia ya kuelekea kwenye eneo la wanawake nilikutana na sura yenye furaha na uchangamfu mkubwa ambayo niliwahi kukutana nayo. Mwanamke huyu wa Kiislam alikuwa na umri sawa na wangu na alikuwa Mmarekani aliyekuwa amesilimu! Sio hilo tu, bali mimi na yeye tulikuwa na majina sawa na tulipo linganisha historia zetu na maisha yetu ya kifamilia kulikuwa na mambo tunayo fanana kabisa. Bila haja ya kusema, hatimaye nilitangaza shahadah yangu na hapo, bila kujua wakati huohuo kwamba mume wangu ajaye alikuwa hapo msikitini, Al-hamdu’lillah.

Miezi kadhaa baada ya kutamka shahadah yangu, nilihisi kuelimika na kuwa madhubuti zaidi katika dini yangu ili hatimaye nitangaze habari hizi kwa baba yangu na mama yangu wa kambo. Baba yangu alijibu kwa kusema kwamba kama Mkiristo mwenye uwezo wa kufikiria sawasawa angeniambia kwamba nilikuwa nafanya makosa… sikujiahangaisha kueleza kuwa haifuati dini yake kwa matendo na kwamba hasira na chuki yake dhidi ya Uislamu na Waislamu inatokana tu na yeye kupotoshwa. Niliuzuia ulimi wangu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Baada ya hapo Baba yangu hakuwasiliana nami tena, lakini mwezi mmoja baadaye nilipomtumia barua pepe kumweleza kuwa nilikuwa nimeolewa, aliniambia kwamba nilikuwa mfu kwake na wala nisiwasiline naye tena. Bado ninamtumia barua pepe mama yangu wa kambo ili kujua hali ya familia yangu lakini kaka, baba, na marafiki zangu wa zamani wamekuwa wakali kuwasiliana nami.

Nimeutumia mwaka uliofuata kujiimarisha na kuendelea katika dini yangu, kupata elimu na maarifa kutoka popote ninapoweza kuipata, na kujaribu kuwafikishia watu ujumbe ambao umenipatia hiyo amani na kuridhika. Niko katika mkakati na mchakato wa kujifunza lugha ya Kiarabu na usomaji wa Qur’an, na kujaribu kuwa mke mwema wa Kiislamu.

Maisha yangu hayafanani hata kidogo na chochote katika maisha niliyoishi kabla ya kusilimu. Sasa hutumia siku zangu katika kudurusu maamrisho ya Mwenyezi Mungu, kuyasoma maisha ya Mtume (s.a.w), na kusoma chochote kinachohitajika ili kuwa Mwislamu mzuri. Nikiwa Mwislamu, napata sana hiyo amani kila siku, kwa kiasi kwamba hata kama mtu anayetenda matendo hayo mema asingelipwa Pepo, bado ningeendelea kushukuru kwa furaha inayopatikana katika misha ya kuishi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Mwanzo nilisema kwamba barabara unayosafiria haionyeshi wapi utakapoishia, na kwamba maisha sio tu kwamba yamejaa maajabu na mambo ya kushangaza bali yanaweza kubadilika yote bila wewe kutambua. Wakati fulani mabadiliko haya yanaweza kuleta majaribu lakini mara nyingi mtu naye ukabiliana vya kutosha na majaribu hayo ubarikiwa zaidi kuliko alivyotegemea. Katika kadhia yangu, nilibarikiwa Uislamu na sio tu maisha bora bali pia tumaini la maisha ya Akhera.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa rehma na ni Mwenye kurehemu.