Madhara Ya Chuki, Uhasidi Na Uadui (Falsafa Binafsi)

Leo nitajaribu kuelezea maradhi makubwa yanayo tusumbua wanadamu wengi kwenye nafsi zetu. Binadamu tunaye adui mkubwa kabisa ambaye tunaishi naye, tunatembea naye na tunalala naye na kushauriana naye kila kukicha. Adui huyu si mwingine ila nafsi zetu wenyewe, hii ni nafsi iliyojaa uadui uwovu na majivuno yakiambatana na kiburi na kutafuta kukomoana, pasipo sababu za maana. Hakuna tabia mbaya katika tabia za binadamu na yenye kuchukiwa kama tabia hii­­.

Tabia hizi kama zikimea kwenye nafsi zetu basi uondoa mfungamano wa kirafiki na kindugu na hata majadiliano yetu hukosa busara na hikma kiasi cha kupelekea kwenye utengano na uhasama.

Mwenye hizi tabia usababisha kufungulia madirisha na milango ya kuchukiwa na watu. Japokuwa kila mtu anatarajia apendwe na aheshimiwe na wengine, ndivyo hivyo hivyo, mtu huyo anategemewa awapende na ahifadhi heshima za wengine pia. Na ajiepushe kabisa na kila jambo linalokwenda kinyume na maingiliano mazuri au yanaosababisha kuharibika kwa maelewano na wengine.

Naweza kuuhita ugonjwa huu kwa jina la maradhi ya kimaadili yanayompata mtu, maradhi haya ya chuki na uadui ni miongoni mwa maafa makubwa ya ufanisi na utulivu wa nafsi, yanaotokana na tabia mbaya ya hasira ya kushindwa katika medani ya kutafuta maisha au kushindwa kwako katika kile unachokitafuta katika kuboresha maisha yako, kiasi ya kuvuruga mtiririko wa fikra chanya na kupelekea kuvuruga uthabiti wa kiroho wa mtu. Huenda ni kutokana na sababu Fulani fulani za kukosea hapa na pale au kujaribu hiki na kile. Kushindwa uku umfanya muhusika kupata hamaki na kujichukia na kupelekea kuwachukia wale waliofanikiwa kimaisha, kiasi ya kwamba kwa wale wasio na uvumilivu uamua kuwasingizia mambo haya na yale wale wanao waona kuwa ni maadui zao. Kiasi ya kusahau kuwa kufanikiwa au kuto fanikia ni mipango yako tu kutokuwa mizuri au kwa kutaka kutumia njia ambazo si za kimaadili, kama vile wizi au utapeli.

Hamaki hizi ni ile chuki iliyojengeka muda mrefu kiasi cha kusababisha moto uliofunikwa chini ya majivu ambao unaweza kutoa cheche za chuki na uadui zitakazounguza na kuteketeza mazao ya ufanisi na utulivu wa nafsi yako.

Bila shaka kutozijali hisia za watu huleta matokeo mabaya ya kudharauliwa na wengine na kuonekana ni mtu duni usiyefaa katika jamii za watu wastaarabu na wasomi.

Kama vile ambavyo kusamehe kunaonyesha utukufu na umakini wa nafsi ya mtu pia kunaleta usalama na umoja na utulivu wa nafsi, vivyo hivyo, uadui na uhasama kunapelekea kuwa na, chuki ambayo uzaa chanzo cha mfarakano na ugomvi. Ingawa uhasama hufanywa ili kutuliza misukosuko ya ndani ya nafsi, lakini madhara anayopata mtu kwa kulipiza ubaya kwa ubaya huwa ni makubwa zaidi kuliko madhara anayopata kwa njia nyingine, kwani maudhi licha ya kuwa ni shida kuvumilia, mwisho wake uondoka, lakini uhasama unapoota mizizi huchoma moyo wa mtu kama miba ya sumu na humkera daima. Isitoshe, uadui hauwezi kuondoa ubaya. Bali hulipanua na kulichimba zaidi donda. Kwa kawaida, uhasama humfanya hasimu ajitetee zaidi na alipize kisasi zaidi, akitegemea kupata utulivu wa nafsi, kumbe ndio anajirimbikizia machungu ambayo umletea maradhi ya saratani ya akili na kupelekea kuwa na maamuzi yasiofaa na yaliojaa visasi na chuki.

Wakati mwingine matokeo ya uadui huwa machungu mno kwa kadiri kwamba huwa hayumkiniki kurekebisha uharibifu unaotokana nao. Huenda mtu katika umri wake wote akaungua moyoni mwake na akaitesa roho yake kutokana na kosa kubwa alilofanya la kuweka chuki. Kutotumia akili na kutofikiria matokeo mabaya ya kufanya ugomvi, akifikiria kwamba anamkomoa mtu kumbe anajikomoa mwenyewe. Maana kila binadamu ana kamusi ya maisha yake na kuna baadhi ya watu, hawana maneno kama vile 'samehe au upendo' kabisa, bali kuna maneno kama vile 'uadui, ugomvi, nitamkomoa, atajuta katika maisha, ataipatapata fresh' na mishabaha na minyambuliko yake ndiyo iliyojaa humo. Kinyongo na hasira kali hutumia nguvu zote katika kulipiza kisasi na kujenga chuki kati ya watu. Tabia ya kupandwa na hasira haraka huandalia uwanja wa chuki. Mtu mwenye moyo dhaifu na mwepesi wa kuhamaki havumilii kusikia akikosolewa au akichambuliwa hata kidogo. Kinyume chake, watu wenye nyoyo safi na madhubuti huchukulia kukosolewa na kuchambuliwa kwao kuwa ni fursa nzuri ya kujirekebisha.

Watu wengi wanashindwa kuelewa kwamba kushikwa na hasira sana ni dalili ya kutopevuka kiakili, kwani huenda mtu anayekosoa huwa hana nia ya kumtukana au kumdharau mwenzake mwenye moyo dhaifu na mwepesi wa kukasirika. Hata kama kitendo hicho kitaonekana ni cha kutukana na kudharau, lakini huenda hakukusudia hivyo. Kwa hivyo, hakuna haja ya kuudhika na kulalamika.

Uchambuzi uliokusudiwa kuudhi na kudharau, kama una ukweli na unaonyesha kosa lenyewe, basi huwa ni zinduo na funzo kwa mwenye akili badala ya kuwa chukio. Lakini uchambuzi usiokuwa na msingi na ukweli usitiwe maanani, kwani unatokana na husuda na ubaya. Kitendo cha kuchambua bila ya msingi wowote ni kitendo cha kitoto, kichuki na kiwivu chenye lengo la kujitukuza kwa kuwadharau wengine. Hata hivyo, tusikereke na watu kama hao, bali tuwafunike kwa shuka ya amani na upendo.

Moyo wa kuweka kisasi na kukomoana ni dalili ya unyonge wa nafsi. Na ni ishara ya maudhi na maonevu aliyoyapata mtu udogoni mwake aidha shuleni, mtaani kwake alipokuwa akiishi au aliyo yaona katika familia au wazazi wake. Mambo haya huweka athari mbaya na kinyongo katika moyo wake kwa kadiri kwamba nafsi yake husumbuliwa na aina moja ya chuki iliyotia fora. Kwa ufupi, kukomoana na kulipiza kisasi ni njia mojawapo wanayoitumia wenye kujihisi duni ili kufidia kushindwa kwao. Hutumia visingizio mbalimbali kuwakera wengine na utenda uhalifu wa hatari kulipiza kisasi kwa yale yaliomsibu alipokuwa mdogo, akitafuta kujifariji ukubwani kwa masahibu ya utotoni. Watu wa aina hii mara nyingi wanakuwa wamelelewa katika koo duni na wakapata vyeo au kusafiri nchi za mbali na kujiona kuwa wao ni bora, hivyo kupelekea kuwa wajeuri. Kwa njia hii hutaka kufidia uduni waliolelewa nao katika koo hizo. Na ujiona ni watu bora kuliko wengine, na hutaka kutumia uhasidi na ubinafsi wao kujitangazia ubora wao. Wengi wetu tunaweza kuwatambua watu wa aina hii miongoni mwetu.

Njia mojawapo ya kuishi kwa amani ni kuwa na utulivu wa moyo na kusahau mabaya ya watu uku ukuzingatia shabaha ya maisha kwa kujaribu au kujitahidi kuishi kwa roho safi na huyapuuza mabaya na upinzani wa kiadui anaokutana nao mtu.

Kila binadamu ana hiari ya kudhibiti taathira ya ubaya katika roho yake, vile vile anao uwezo wa kubadilisha jambo baya kuwa zuri au fikra mbaya kwa fikra nzuri na kujibu ubaya kwa uzuri. Kwa hivyo, tunaweza kupunguza nguvu za taathira mbalimbali juu ya fikra zetu kwa kutegemea nguvu za matakwa yetu, na kwa njia hiyo tukapata nguvu za kutosha kuweza kuvunja hisia ya chuki ambayo huzisumbua roho zetu. Hakuna mtu atakayeweza kutusaidia tutakapo shindwa kutekeleza wajibu wetu zaidi ya mtu binafsi mwenyewe.

Kukomoana na kuzushiana mambo yasio mazuri, kama vile vifo au uhalifu ni mambo ambayo si katika ubinadamu, watu wa namna hii ujificha katika ngozi tofauti tofauti. Baadhi ya watu huvaa ngozi za urafiki au uswahiba au kujionesha kuwa ni mpenda dini na haswa hizi zama za utumiaji wa mitandao, watu uweza kukuomba urafiki na kuwaongeza kwenye orodha ya watu utakaokuwa ukiwasiliana nao au wengine ujitia kwenye siasa na kujifanya kuwa wao ni wapinzani, kumbe ni wanafiki na kuchukuwa siri za wengine kisha kuwachongea na kwa njia hii wanaweza kuwakomoa au kuwaangamiza wengine kisiasa au kiuchumi na katika jamii kuonekana kama ni wasaliti.

Niliwahi kusoma sehemu zamani kuwa:
“Chuki na uadui ni matokeo ya upumbavu hasa panapokosekana sababu maalumu. Tunaweza kuyatatua mambo mengi kwa urafiki, lakini ubinafsi hautuachii. Hutokea mara nyingine tukavunja urafiki kwa sababu ya adha ndogo kabisa, wakati tunaelewa kwamba kosa lao ni kuwa na imani tofauti na yetu au wakati mwingie wanaunga mkono fikra tofauti na sisi. Kwa kweli, tunashindwa vipi kuvumiliana katika mustakabari wa maisha yetu na hali sote tuna haki ya kuamini na kufuata fikra tunazo amini kuwa zitatukomboa kimaisha...!?”

Watu hawa wapo tayari kupoteza muda na wakati wao na nguvu zao katika kujitengenezea maadui, uku wakijikomba kwa watu (matajiri, watawala au wanasiasa) wanao amini kuwa wanaweza kuwasaidia katika kutatua maisha yao waliyo yaharibu kwa uhalifu wao. Hali hii uendelea mpaka pale hasidi huyu atakapo fanikiwa, ingawa ni mara chache sana kufanikiwa, lakini hata atakapo fanikiwa hakumpi utulivu wowote wa nafsi na matokeo yake umpelekea kutafuta adui mwingine na mwingine mpaka kumpelekea kupata maradhi mabaya ya nafsi na kuanguka kwa aibu.

Wengi wetu tunashindwa kuelewa kuwa mapenzi ya kijamii ni sababu muhimu kabisa ya mtu kupata maendeleo na mafanikio mazuri katika maisha yake. Mtu mwenye mapenzi na watu akaishi kwa wema na upendo kiasi ndio zikawa sifa zake, basi mtu huyu anayeweza kutawala hata nyoyo za watu na kupanda ngazi ya maendeleo kwa kunufaika kwa msaada na ushirikiano wa jamii na kupata ufunguo wa mafanikio. Mtu mzuri kwa tabia na amali ni kama taa inayong'aa yenye kuongoza fikra na maendeleo ya jamii. Usafi wake wa moyo una taathira kubwa katika muundo wa maadili ya watu.

Kwa kuwa kijicho kina sura mbaya, hivyo hujitangaza chenyewe kuwa ni adui wa tabia na sifa nzuri na kizuizi kati ya watu. Kijicho hakimpi mtu fursa ya kupendwa na watu anao ingiliana nao. Hivyo, mwenye kijicho hukosa fursa za ushirikiano na neema ya mapenzi. Hasidi huonyesha waziwazi ubaya wake unaotokana na vitendo vya tabia yake mbaya, na kwa sababu hiyo hulaaniwa na huchukiwa sana na watu. Na kupelekea kupata huzuni ambazo huingia moyoni mwake kutokana na uhasidi wake, kiasi huikandamiza roho yake katika moto mkali na kuteketeza maisha yake.

Siku zote moyo wa mwenye wivu, husda na roho mbaya, daima uona uchungu na uwa hauna raha wakati wowote. Kwa sababu anaishi kinyume na imani yake, kwa sababu ya kuikataa neema za Mwenyezi Mungu hambazo hazina kikomo, hivyo uishi kwa mashaka na wasiwasi kwa sababu hiyo zile kutu za huzuni huwa haziwezi kutoka kabisa katika moyo wake mpaka anaingia kaburini.

Hali hii ya uhasidi ikishamiri katika jamii, basi upelekea migogoro na ugomvi wa kila aina. Mazingira kama hayo yanayochafuliwa na ugonjwa wa chuki na roho mbaya ya uhasidi huwa ni kizuizi mbele ya maendeleo si ya mtu mmoja mmoja tu, bali jamii kwa ujumla, hivyo kuvuruga nidhamu ambayo ni kiini cha maendeleo ya watu na kusababisha maanagamizi ya jamii hiyo akiwemo hasidi mwenyewe.

Kila mtu au binadamu ana haki ya kuheshimiwa katika jamii kwa kadiri ya heshima na hadhi yake. Mtu anayejifunga katika kuta nne za majivuno na nafsi yake ikatawaliwa na chuki, hatajali kamwe kuwaaribia wengine isipokuwa atazingatia matakwa yake tu. Kwa hivyo, atajaribu kwa nguvu zote kuwaudhi na kuwakera wengine na kujifanya mashuhuri na msifiwa, na kuilazimisha jamii imuone yeye ni bora.

Dhana mbaya ni athari isiyozuilika katika nafsi ya hasidi. Miali ya moto ya mwenye dhana mbaya ya kujiona daima huwaka na huwadhania wote kuwa ni wenye kumchukia na kumtakia mabaya.

Kudharauliwa kwake na kupata mapigo ya daima kutokana na maringo yake hakumsahaulishi kamwe ubaya wake. Bali uendelea kutafuta mbinu hizi na zile kiasi ya kwamba kichwa chake husumbuliwa na fikra zake bila ya mwenyewe kutaka. Na kila akipata fursa hutaka kuifanyia chuki jamii, na uwa hawezi kuona raha madhali machafuko na machemko ya ndani mwake hayajatulia.

Kirusi cha majivuno na maringo hutokeza katika dhamiri ya mtu baada ya kuugua maradhi ya kinafsi ya kujihisi duni. Maradhi hayo hugeuka kuwa kirusi duni ambacho kwa sababu ya kuwa kiharibifu na chauma, huenda kikawa ni chanzo cha hatari nyingi na uhalifu wa kila aina. Kirusi hiki duni humfanya mwenye kujinata afanye ukatili na udhalimu.

Mtu mwenye thamani na hadhi ya kweli hatakuwa na haja ya kujivuna au kujionyesha mbele ya watu wakati wowote ule, kwa sababu anaelewa vyema kwamba kujiona si msingi wa ubora, na roho mbaya haimfai mtu yeyote wala haimfikishi mtu yeyote kwenye kilele cha utukufu na ufakhari.

Basi nadiriki kusema kwamba, kumdharau mtu mpumbavu na kujiepusha na marumbano yasio na tija ni fimbo tosha kabisa, kwa sababu ukiingia wenye marumbano na mtu mpumbavu atakushusha hadi ufikie upeo wake wa kufikiri kijinga na kipumbavu, na kisha atataka kukugaragaza kwa upumbavu wake, na kwa sababu hana hoja, mwishoni utashindwa kuendelea naye... Lakini ukiingia kwenye marumbano ya hoja dhidi ya wasomi, ukiwashinda au wakikushinda basi utafaidika kwa elimu yao, kwa sababu wana upeo unao lingana na wewe, na hapo lazima utaondoka na faida japo mbili au tatu.

Siri moja kubwa sana ya kumuumiza mtu mpumbavu kisaikolojia ni kumdharau na kumfanya kama hayupo, yeye mwenyewe ndio atakuwa akiangaika, maana hajui umeuchukuliaje upumbavu wake.

Kila mtu ana mwendo wake maalumu unaotokana na hali yake ya kimaadili na kinafsi. Msamaha ni mojawapo kati ya sura angavu kabisa ya utukufu na udhibiti wa nafsi, na ni aina moja ya ushujaa na uungwana. Mwenye kuwa na sifa hiyo kwa kadiri ya kutosha na mbali ya kuwa na nguvu na uwezo wa kulipiza lakini akasamehe, hufaidika kwa kuwa na uhakika na usafi wa moyo ambao hauwezi kulinganishwa na kitu chochote kingine. Kusamehe kunaitukuza na kuiimarisha roho ya mtu, na ni kipawa ambacho kwacho hububujika upole na wema. Kusamehe humtoa mtu kwenye kifungo cha ubinafsi. Ingawa ni shida sana kusahau madhara na mabaya ya wengine na moyo huumia sana mwanzoni, lakini kwa kadiri mtu atakavyovumilia katika njia hiyo ndivyo atakavyoweza kupunguza sana masumbufu yake ya rohoni na mwisho wake akawa ni mtu msamehevu na aliye bora kabisa katika jamii.

Hapana shaka kwamba kusamehe kunaweka athari nzuri katika moyo wa adui kwa kadiri kwamba uweza kuleta mabadiliko katika fikra na mwendo wake. Chuki nyingi zimeondoshwa kwa kusamehe, na uadui mkali na wa kizamani umeondoshwa na mahali pake kukaa usafi wa moyo na upendo. Adui mchokozi hulainika na husalimu amri mbele ya mtu aliyejizatiti kwa silaha hii kali na kwa fikra za kiungwana.

Jambo la kuzingatia:
Kimojawapo kati ya vipawa vikubwa kabisa vya binadamu ambavyo wanyama wengine hawakufaidika navyo ni hisia ya kusamehe makosa ya wengine. Mtu anayekuudhi huwa kwa wakati huohuo hukupa fursa nzuri ya kumsamehe na kuona utamu wake. Tumefunzwa kuwasamehe maadui zetu lakini hatukuambiwa tusiwasamehe marafiki zetu. Hivyo, ni wazi kwamba ni lazima tusahau mabaya tuliyotendewa na wengine. Unapomlipizia kisasi adui wako huwa ni sawa naye, lakini unapomsamehe wewe huwa ni bora kuliko yeye, kwani yeye huwa ni mwovu, nawe huwa ni msamehevu. Huenda tusifanikiwe tunapotaka kulipiza kisasi, lakini kusamehe ni njia bora kabisa ya kulipiza kisasi. Kwa kusamehe tunaweza kuwashinda maadui zetu bila ya kupigana na kuwafanya wainamishe vichwa vyao mbele ya utukufu wetu. Kwa hivyo, kuacha chuki na kukwepa uadui ni shambulio kubwa kabisa lenye kuwashinda mahasimu wetu. Tunapotendewa maovu, tuwatendee mema, kwani kulipa mema kwa mabaya uliyofanyiwa ni siasa ambayo kwayo hupatikana amani duniani.”

0 comments/Maoni: